Na Gift Mongi
Moshi
KIKUNDI cha Kwaya ya Mtakatifu Agustino Cha Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mume wa Bikira Maria lililopo Mwenge – Longuo Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Jumapili tarehe 30.06.2024 kulifanyika uzinduzi wa albamu yake ya kwanza yenye nyimbo 10. Jina la Album hiyo ni TETEA IMANI.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mume wa Bikira Maria Padri Richard Temba alimshukuru sana Mbunge Ndakidemi kwa kuacha shughuli zake zote na kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa album ya kwanza ya kwaya ya Mtakatifu Agustino iliyopo hapo Parokiani.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kanisani hapo, mgeni rasmi na familia yake aliichangia kwaya hiyo Sh milioni moja na laki tano kwa ajili ya kuendeleza kikundi hicho kinacho Injilisha kwa njia ya Nyimbo
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mbunge aliwapongeza sana wana kwaya hao kwa kuamua Kumtukuza Mungu kwa KUIMBA.
Vilevile aliwapongeza kwa huduma nzuri wanazotoa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimba kanisani, kuimba katika misa za ndoa, sendoff na misa za mazishi.
“Naomba akina baba mjiunge na kwaya hii kwani imeelezwa kuwa kuna idadi ndogo sana ya waimbaji wanaume alisema Ndakidemi”.
Aliwashukuru sana kwa kumshirikisha katika shughuli hiyo Muhimu ya Kiroho.