Rais wa Iran Ebrahim Raisi, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo na wengine wamepatikana wakiwa wamekufa katika eneo la ajali ya helikopta,kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya serikali. Raisi alikuwa na umri wa miaka 63.
Vyombo vya habari vya serikali havikutoa sababu za haraka za ajali hiyo. Watu wote tisa waliokuwa kwenye helikopta hiyo walifariki wakati ilipoanguka katika jimbo la kaskazini-magharibi mwa Azerbaijan la Iran.
Raisi na waziri wa nambo ya Nje Amir Abdollahian walikuwa wakisafiri kurudi kutoka mkutano na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev. Helikopta hiyo ilitoweka kwenye rada Jumapili mchana.
Shirika la habari la Iran la Mehr nalo limelipoti kwamba “Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatollah Ebrahim Raisi, alipata ajali akiwahudumia na kutekeleza wajibu wake kwa ajili ya watu wa Iran na amekufa shahidi.”
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kwamba hapakuwa na mtu aliyenusurika katika eneo la ajali.
Serikali bado haijatoa taarifa rasmi ya kuthibitisha ripoti hizo.
Hapo awali, televisheni ya taifa ya Iran, ilisema timu za waokoaji zinatajwa kuyafikia mabaki ya helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi na maafisa wengine.
Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa “hakuna dalili ya mtu aliye hai” katika eneo la ajali ya helikopta iliyombeba Rais Ebrahim Raisi na wengine.
“Baada ya kupata helikopta hiyo, hapakuwa na dalili zozote za abiria wa helikopta kuwa hai hadi sasa,” imeongeza ripoti hiyo.
Mkuu wa shirika la Hilali Nyekundu la Irani Pirhossein Koolivand amesema “helikopta hiyo imepatikana” na kwamba timu za uokoaji zilikuwa zikisogea karibu na eneo la ajali. Koolivand aliongeza kuwa “hali haikuwa nzuri.”
Helikopta hiyo iliyombeba Raisi, ilianguka katika eneo la mbali kaskazini mwa Iran Jumapili jioni kutokana na hali mbaya ya hewa.
Hali mbaya ya hewa katika eneo hilo inatajwa pia kutatiza shughuli za utafutaji huku rais akiwa ametoweka kwa zaidi ya saa 12 kufikia mapema Jumatatu.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kwamba waliokua safarini na rais katika helikopta hiyo ni waziri wa mambo ya nje wa Iran Hussein Amirabdollahian, Gavana wa jimbo la Azerbaijan Mashariki Malek Rahmati na abiria wengine kadhaa.
Taarifa za awali
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Iran, helikopita hiyo imepata ajali karibu na eneo la Jolfa, zaidi ya kilomita 600 kutoka Tehran karibu na mpaka na Azerbaijan.
Ziara ya Rais Ebrahim Raisi Afrika ilitafuta uungwaji mkono?
Nchi kadhaa zikiwemo Urusi na Uturuki zimetoa msaada katika operesheni ya uokoaji, huku ndege isiyo na rubani ya Uturuki pia ikiruka katika anga ya Iran kusaidia shughuli ya utafutaji. Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amewatolea mwito Wairan kumwombea Raisi.
Raisi aliapishwa kama rais mpya wa Iran mnamo Agosti 2021. Alishinda uchaguzi wa urais mwezi Juni na chini ya asilimia 62 ya kura kama mgombea mkuu wa vyama vya siasa kali na anayependwa zaidi.
Alizaliwa mwaka wa 1960 huko Mashhad, kaskazini-mashariki mwa Iran, Raisi anazingatiwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Anadumisha uhusiano wa karibu na Khamenei.
Kwa mujibu wa katiba, Raisi ni kiongozi nambari mbili nchini Iran, akimfuata Khamenei aliye mkuu wa nchi na pia ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati.