SERIKALI inatarajia kuanza kukagua matumizi ya Sh.bilioni 9.6 zilitolewa ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuhudumia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA’s) baada ya kubaini kuwapo kwa ufujaji.
Akizungumza jijini hapa kwenye kikao cha viongozi jumuiya hizo na baadhi ya maofisa wanyamapori kuhusu kero za usimamizi wa maeneo hayo nchini, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema fedha hizo zilitolewa kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo ya vijiji.
Amefafanua kuwa fedha hizo zilielekezwa kwenye WMA 22 zilizoidhinishwa na kupata haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori na kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo hali inayolazimu serikali kufanya ukaguzi.
“Mjiandae tunajipanga kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali, fedha hizo si za viongozi wala mtu binafsi, mnapaswa kuwa na matumizi bora ya fedha na yenye uadilifu,” amesema.
Kuhusu mikataba wanayoingia, amewataka iwe yenye tija kwa maslahi ya Taifa ambayo haitasababisha migogoro kwenye jumuiya hizo za hifadhi.
Hata hivyo, amesema kumekuwapo na migogoro ya mipaka baina ya WMA na hifadhi zingine hali inayochangia kupunguza ari ya uhifadhi kwa wananchi.
Amesema migogoro mingine ni baadhi ya maeneo ya WMA kuvamiwa na mifugo, hivyo kupunguza tija katika uhifadhi na kuzorotesha uwekezaji katika maeneo hayo.
Amesema: “Kuna baadhi ya WMA’s zinakosa mapato kutokana na kukosa wawekezaji. Mfano hadi sasa takribani WMA’s tisa hazina mapato kabisa kutokana na kukosekana kwa uwekezaji, ninaamini changamoto hizo na nyingine nyingi mtakazoziwasilisha leo kupitia kikao hiki zitatafutiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano au kuhitaji mapitio au maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia uhifadhi nchini”.