Tabora ni moja ya mkoa unaopatikana upande wa magharibi mwa nchi ya Tanzania. Ni miongoni mwa mkoa mkubwa nchini Tanzania. Ukiwa mkoani Tabora unaweza kufika kwenye wilaya zenye historia na vivitio vya utalii kama wilaya ya Sikonge, Uyui, Urambo, Nzega, Kaliua, Igunga Na Manispaa Ya Tabora Mjini.
Makabila yanayopatikana mkoani Tabora ni Wanyamwezi ambao ndio wenyeji huku makabila kama Wasukuma, Waha na makabila mengine wakiwa kama wageni. Ukitoka mkoa wa Dar Es Salaam, kuna umbali wa kilomita zaidi ya 800 kufika mkoani Tabora. Na unaweza kufika mkoani Tabora kwa usafiri wa mabasi, ndege na treni. Wakazi wa mkoa huu wanalima sana tumbaku na baadhi ya mazoa ya chakula na biashara.
Pia kuna wafugaji ambao hufuga kama sehemu ya biashara na tamaduni. Hali ya hewa ni nzuri ambapo kuna joto kiasi kipindi cha kiangazi na hali ya ubaridi kipindi cha masika. Wakazi wa Tabora hupendelea sana vyakula kama viazi, wali na ugali huku wakitumia sana karanga kama sehemu ya kiungo cha mboga. Pia mkoani Tabora kuna matunda ya aina mbalimbali yenye kupendwa na wakazi wa mji wa Tabora.
Na mara baada ya kufahamu machache kuhusiana na mkoa wa Tabora, ni wakati sasa wa kufahamu historia ya asili ya jina Tabora. Ifahamike kwamba, katika miji mingi iliyopo hapa barani Afrika asili ya majina yao yametokana na uwepo wa lugha za kikabila na baadhi ya miji majina yao yametokana na ujio wa wageni. Kama ilivyo katika historia ya mji wa Mtwara kuwa asili ya jina hilo linahusiana sana na lugha ya kimakonde.
Na hata kwa upande wa Tabora asili ya jina hilo linahusiana sana na lugha ya kinyamwezi. Historia inasema hivi wakati Waarabu wanafika katika mji wa Tabora mnamo miaka ya 1830 walikuta mji huo umeendelea hasa katika maeneo ya Kwihala na Itetemya. Na hii ni kwa sababu kuwa, maeneo hayo yalikuwa yana idadi kubwa ya watu.
Waarabu hawakuwa na mpango wa kukaa hapo, ila kwa kuwa walirazimishwa kutoa kodi na ndipo walipoaanzisha vita na mwisho kuchukua maeneo hayo na kujenga tembe ambalo lipo pale mpaka leo.
Na mara baada ya Waarabu kukaa hapo, kuliibuka baadhi ya Waarabu ambao waliokuwa maarufu sana kama wakina Kazeh. Na Kwa kuwa mtu huyo kumwakilisha Sultani wa Zanzibar, alitokea kuheshimiwa sana na wakazi wa Tabora.
Na hata yale maeneo aliyokuwa anakaa yalijulikana kama kwa Kisehi (jina lilitamkwa kimakosa). Na mpaka wamishionari na wapelezi wanafika katika mji wa Tabora kama wakina Dr.livingstone na Henry Stanley waliufahamu mji wa Tabora kwa jina la kwa Kisehi ambapo kwa Waarabu alifahamika kama Kazeh. Hivyo mji wa Tabora ukafahamika kama Kazeh kulingana na ujio wa wageni hao.
Lakini ikumbukwe kuwa utamaduni wa wenyeji kwa wakati ule na hata sasa, ulikuwa unategemea sana kilimo cha viazi vitamu. Baada ya kuvunwa viazi hivyo vinachemshwa na kisha kukatwa vipande na kuanikwa. Zao litakalopatikana baada ya mchakato huo linajulikana kwa kinyamwezi kama matobolwa.
Hivyo mwingiliano wa Wanyamwezi, Waarabu pamoja na Waswahili kutoka Pwani ndio kulileta ugeuzi wa matamshi hayo kutoka “matoborwa” “matohorwa” na kuwa Tabora. Hivyo neno Tabora limetokana na kushindwa kimatamshi kwa baadhi ya wageni .
Hivyo wengi walianza kusema, “twendeni kwenye mji wa matoholwa” na mwisho wa siku binadamu anaamua kurahihisha matamshi na kuwa “twendeni Tabora” na hivyo ndivyo jina Tabora lilivyopatikana. Na leo hii ukiwa mjini Tabora utapata kusikia sehemu panaitwa “Kazeh hill” wakimaanisha sehemu ambayo liwali Kazeh alipokuwa anakaa.
Leo hii Tabora ni moja ya mkoa wenye kubeba historia kubwa sana, ukizungumzia historia ya TANU huwezi kuacha kutaja mji wa Tabora. Na pia mkoa wa Tabora ni moja ya mkoa wenye vivutio vingi sana, kuna makumbusho ya Kwihala, kuna misitu ya asili,kuna mabonde na milima yenye kuvutia, kuna mito mbalimbali na bila kusahau ukiwa wilayani Sikonge kuna kaburi la mchungaji wa kwanza wa kinyamwezi wa kanisa la Moraviani.
Na pia utapata kuona kanisa la pili la Moraviani lililojengwa miaka ya 1897 na linatumiaka mpaka leo. Lakini pia utalii wa kiutamaduni unapatikana sana mkoani Tabora hasa kwa makabila kama Wanyamwezi na Wasukuma. Hakika mkoa wa tabora ni urithi wetu. Maandiko haya ni sehemu tu ya historia ya Tabora, bado mawazo yako yanahitajika sana.