You are currently viewing MNYIKA AOMBA MAONI KWA WANACHAMA MWALIKO MAREKEBISHO YA KANUNI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

MNYIKA AOMBA MAONI KWA WANACHAMA MWALIKO MAREKEBISHO YA KANUNI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amewaomba Wanachama wa CHADEMA watafakari kuhusu mwaliko wa kikao cha kupitia na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ambao Chama hicho kimepewa na wawape Viongozi maoni na ushauri wa haraka juu ya hatua za kuchukua, hii ni baada ya mwaliko huo kutoambatana na nakala ya rasimu ya kanuni tajwa.

Mnyika ametoa taarifa hiyo leo June 12,2024 kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), ambapo ameandika “Amani iwe nanyi, kwa Wanachama wote CHADEMA naomba kuwataarifu kuwa jana tarehe 11 Juni 2024 tumepokea mwaliko wa kikao cha kupitia na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, hata hivyo mwaliko wa kikao hicho cha tarehe 15 Juni 2024 kilichopangwa kufanyika Dodoma haukumbatana na nakala ya rasimu ya kanuni tajwa”

“Tumetaka nakala ya rasimu ya Kanuni hizo kutoka kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mpaka leo hatujapewa, kwakuwa uchaguzi huu unahusu mitaa na matawi ya Chama Tanganyika nzima sanjari na umma tunaowaongoza nimeona niwaandikie ujumbe huu ili mfahamu na mtafakari kuhusu mwaliko na mchakato huu unaoendelea na mtupe maoni na ushauri wenu wa haraka juu ya hatua za kuchukua nikizingatia kuwa Chama ni wanachama, vikao na uongozi”

“Nasubiria mrejesho wenu kwa wakati nikiwatakia heri katika majukumu yenu na mapambano ya haki, uhuru, uadilifu, demokrasia na maendeleo ya Watu”

Leave a Reply