Na Gift Mingi
Moshi
Mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Mandaka Mnono uliopo katika jimbo la Moshi Vijijini unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.1 umetajwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo mara baada ya kukamilika kwake.
Haya yanatokea katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayofanywa na mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi katika kata ya Oldmoshi Magharibi na kukagua Ujenzi wa mradi wa huo.
Ziara hiyo ambayo ilijaa matumaini Prof Ndakidemi aliambatana na viongozi kadhaa wa chama cha mapinduzi(CCM)ngazi ya wilaya wakiwemo katibu wa CCM wilaya, Ramadhani Mahanyu, katibu wa wazazi wilaya Andrew Mwandu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya vijana wilaya, Yuvenali Shirima, Peter Massawe (Diwani wa Kata), Christina Mchau na Jennifer Chuwa (Madiwani wa viti maalumu), na viongozi wa CCM na Serikali Kata ya Oldmoshi Magharibi.
Aidha katika kupokea taarifa ya mradi huo kuliibuka baadhi ya changamoto ambapo kubwa iliyopo ni katika ngazi ya usanifu, mradi huo haujaweka kipengele cha kusawazisha eneo (levelling) eneo lote la Mradi, jambo ambalo huko mbeleni litasababisha tatizo la kufikisha maji kwenye mashamba kutoka mfereji mkuu.
Hata hivyo mbunge aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika Kata ya Oldmoshi Magharibi kwa kipindi cha miaka minne tokea aingie madarakani katika mkutano wa hadhara na wananchi.
Aliainisha miradi yote ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye Kata ya Oldmoshi Magharibi ambapo jumla ya Shilingi bilioni 6,644,359,294.00 zimetumika katika miradi ya Kilimo, Maji, Elimu, Barabara, Afya, na Mikopo kwa Jamii.
Baadaye, wananchi walipata fursa ya kumweleza Mbunge kero zao huku kubwa zilihusisha Ubovu wa Barabara na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha chini, Matumizi ya changarawe zenye kiwango duni, ukosefu wa maji katika Zahanati ya Mandaka Mnono na Vitongoji vya Uswahilini.
Kero nyingine ni uharibifu na ujenzi holela katika vyanzo vya maji katika maeneo yote ya Kata, Uchakavu wa Madarasa katika Shule ya Msingi Maringeni, ukosefu wa Maabara katika Zahanati ya Tela na Shule ya Sekondari Maringeni, Uchakavu wa Mifereji ya Asili na usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo ya Serikali inayotekelezwa katika Kata.
Mbunge alishauriana na Diwani, akajibu kero zote na kuchukua kero zile ambazo hazikuwa na majibu na kuwahakikishia wananchi kuwa atazipeleka kwenye mamlaka husik na baadaye Mbunge aligawa miche bora ya migomba.
Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya, Katibu wa CCM wilaya Ramadhani Mahanyu alimshukuru Mbunge na Diwani kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea wananchi wa Oldmoshi Magharibi miradi mikubwa ya maendeleo.
Aliwashauri Wana Oldmoshi Magharibi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge Ndakidemi na Diwani Massawe kwani kazi walizofanya ni kubwa na zenye tija na Wananchi kwa ujumla wanasonga mbele kimaendeleo kuwaasa vijana kuachana na tabia ya ulevi uliokithiri.
Mwisho