You are currently viewing MIAKA 40 BILA SOKOINE: Ujue upekee wake Edward Sokoine

MIAKA 40 BILA SOKOINE: Ujue upekee wake Edward Sokoine

Na. Nipashe Publisher

  1. Edward Sokoine, alipokuwa akiteta jambo na Rais Julius Nyerere.
    LEO inatimu miaka 40 tangu kufariki aliyekuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza, Edward Moringe Sokoine, mwaka 1984.

Hulka na nafsi yake;

  1. Amekuwa muumini wa Haki, Usawa na Uwajibikaji.
  2. Ameamini katika itikadi na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
  3. Kiitikadi akazama katika msimamo kwamba, maendeleo huja kwa watu kujituma kufanya kazi halali na bidii.
  4. Pia, aliamini katika mabadiliko chanya kwa jamii yake.
  5. Mara zote akawa mzalendo hasa kwa taifa alilotumikia maisha yake yote.
  6. Amechukia vitendo vya rushwa, hujuma, uhujumu uchumi, ulanguzi na magendo.
  7. Alikuwa mtu wa vitendo na kamwe alikuwa si mtu wa kupenda kulalamika lalamika.

Mchango wake kitaifa;

  1. Siku zote akawa mstari wa mbele enzi za vita ya Kagera kupambana na Nduli Idd Amini Dada, aliyetangaza kuteka sehemu ya mkoa wa Ziwa Magharibi, iwe sehemu ya taifa la Uganda.
  2. Alianzisha vita dhidi ya Uhujumu Uchumi nchini, biashara ya ulanguzi, magendo na aliichukia rushwa kwa vitendo
  3. Mara zote akabaki mzalendo wa kweli wa taifa hili.
  4. Amedumu akisimama katika msimamo ‘siasa ni kilimo’, akiamini ‘kilimo ni uti wa mgongo wa taifa’, hata kifo chake kilitokea katika hatua ya kuacha kusafiri kwa ndege, ili impe fursa kushuhudia kinachoendelea mashambani na ustawi wake, kutoka juhudi za Watanzania walioko katika sekta hiyo kuu.
  5. Alitunza na kutukuza utamaduni wa Kiafrika na utaifa wa Mtanzania.

SAFARI YAKE KISIASA

Mnamo Januari 1,1961, akiwa kamaliza elimu ya sekondari, Edward Moringe Sokoine alijiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ikiwa ni miezi michache kabla Tanganyika haijapata Uhuru.

Akiwa mwanachama hai wa TANU, mwaka 1962, alienda Ujerumani Magharibi (sasa zimeungana), ikiwa rafiki wa taifa jipya la Tanganyika, Sokoine akaenda kusomea fani ya Utawala na aliporejea mwaka 1963, alipangiwa kazi Ofisa Mtendaji wa Wilaya (DEO), wilayani Masai, hata akafana kikazi ambako kulikuwa kwao.

Mnamo Septemba 30, 1965, akiwa kijana mdogo wa miaka 27, aliyeonyesha akili na ubunifu mkubwa, akagombea ubunge jimbo la Masai na kumshinda kwa kishindo mpinzani wake, Edward Carli Boniface Ole Mbarnote, aliyekuwa Chifu wa Wamasai. Sokoine alitwaa kura 6,977, Chifu Mbarnote akiambulia kura 871.

Akiwa bungeni, nako akaonyesha umahiri wa uwakilishi wake, kwa umahiri na stadi za uwakilishi, ikiwamo kudai sababu za Wamasai wa Ngorongoro kuzuiwa kulima, wakati hawana mifugo inayowalisha.

Ni sehemu ya maono yaliyomfanya kuaminika maradufu mbele ya Rais Julius Nyerere, aliyevutiwa naye, japo katika umri mdogo.

Katika hali iliyoonyesha kuaminika mwaka 1967, Mwalimu Nyerere akamteua kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi n Mwaka 1970, akamteua kuwa Waziri wa Nchi, huku mwaka 1972, Rais Nyerere akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Hata katika ulingo wa kisiasa, heshima na chati yake ilipanda maradufu, pale vyama TANU na Afro Shiraz Party (ASP) kuungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Februari 5, 1977, Sokoine akateuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ambacho ni cheo chenye hadhi nyeti katika siasa ya nchi tangu zama hizo, akidumu nacho hadi kifo chake, siku kama ya leo, mwaka 1984.

Katika vita vya Kagera mwaka 1979, akiwa Waziri Mkuu, Sokoine alikuwa kiungo muhimu, hata mwanzoni mwa vita hivyo, akiwaagiza wakuu wa mikoa wote wakusanye nyenzo zote tayari kwa vita ya kupambana na Nduli Idi Amin Dada wa Uganda.

Binafsi, mnamo Januari 23, 1979, akatembelea eneo la vitani mpakani Mutukula (sasa wilaya ya Misenyi) kukagua hali ya usalama na inaelezwa wakati wote wa vita, Sokoine alikuwa ni nadra kulala usingizi, hali inayotajwa hata kuchangia mtetereko wake kiafya.

Novemba 1980, kukafanyika uchaguzi nchini, Sokoine aliomba na kukubaliwa kujiuzulu uwaziri mkuu, akaenda nchini Yugoslavia kwenye matibabu, nafasi yake ikashikwa na Cleopa David Msuya.

Baada ya kurejea, Mwalimu Nyerere akamteua tena kuwa Waziri Mkuu Februari 24, 1983 na mwaka huo huo akiendeleza masomo yake ya Shahada ya Sayansi ya Siasa.

MWASISI WA DALADALA

Katika miaka ya 1980, nauli ya daladala ilikuwa Sh. tano na safari zake ni za ‘kuiba’, huku mitaa yote ikitawaliwa na mabasi rasmi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Kukua kwa jiji la Dar es Salaam, ikalemewa katika utoaji huduma. Sokoine akiwa Waziri Mkuu, akaamuru magari binafsi yaanze kuisaidia UDA kubeba abiri kwa nauli ya shilingi tano na kwa kuwa kiasi hicho cha pesa kimedumu kuwa na jina la mtaani ‘dala’ basi ikawa jina la mabasi binafsi ‘Daladala.’

VITA VYA UHUJUMU UCHUMI

Aprili 5, 1983, Mwalimu Nyerere. Ndiye aliyezindua kampeni ya kupambana na wahujumu uchumi baada ya kupitishwa kwa sheria yake mwaka 1983, ambayo ikamea sana, ikiwamo kupitia redioni.

Ni sheria inayomtaka mtu aeleze mali zake, huku kukiwapo mahakama yake maalum, ambayo ilikuwa na vipengele vya masharti.

Utekelezaji wa kampeni hiyo, baadhi ya washukiwa katika sehemu nyingi nchini, hasa Dar es Salaam, walihofu sana na kutupa barabarani na mitaroni.

Hivyo ni vitu vya thamani vilivyoingizwa nchini kinyemela, kukiwapo simulizi ya kutupwa mabunda ya fedha na mali kama televisheni. Polisi wakaziokota na kuzikabidhi kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ni wakati sheria za nchi hazikuruhusu mtu binafsi kuwa na maduka makubwa ya jumla, kazi iliyofanywa na Shirika la Biashara la Mkoa RTC

Ni rekodi iliyoacha, jina lake Sokoine likapaa maradufu hata kumjenga sana kisiasa, akapendeka zaidi kitaifa.

· Kwa mujibu wa ushuhuda, historia na michango ya uchambuzi.

emmanuel

Komkya Nexus---- Komkya Nexus is a dynamic platform dedicated to delivering the latest in media updates, insightful blogs, and comprehensive business solutions. Our mission is to keep you informed and help your business thrive with expert content and innovative services. Join us and stay ahead in the ever-evolving world of media and business.

Leave a Reply