You are currently viewing NDOTO YA W.O.P ILIVYOTIMIZWA NA SERIKALI

NDOTO YA W.O.P ILIVYOTIMIZWA NA SERIKALI

Na Gift Mongi
Dar es Salaam

Kwa kipindi cha hivi karibuni viwanda vinavyojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa mbali mbali kwa kutumia malighafi ya ngozi vilipita katika kipindi kigumu.

Naam ni kweli kipindi kigumu kutokana na kile ambacho kilielezwa ni biashara hiyo kuonekana kuwa ni ngumu au kwa kuingiliwa kutokana na uingizwaji wa bidhaa hizo kiholela kutoka nje ya nchi.

Kuingizwa kwa bidhaa hizo kulipelekea zile zinazozalishwa hapa nchni kushindwa kuhimili soko la ushindani kutokana na sababu mbali mbali

JE HALI ILIKUWAJE?

Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi kijulikanacho kama Woisso Original Products (WOP)Kenneth Woisso alisema kuwa kuingizwa kwa bidhaa hizo kuliwafanya kushindwa kuzalisha kwa kasi na kwa kiwango kama ilivyokuwa hapo awali.

Alisema bidhaa hizo ambazo zilikuwa na mfanano wa ngozi lakini sio ngozi vilevile ni kama zilikuwa zikiwaharibia soko kwani mteja alishindwa kutofautisha ngozi halisi na ambayo ni bandia

Vilevile katika soko zenyewe ziliuzwa kwa bei ya chini kidogo ikilinganishwa na zile ambazo zinazalishwa hapa nchni hivyo wateja wengi kuzikimbilia kutokana na unafuu wa bei

JE ALITAMANI NINI KIFANYIKE?

Alisema alichokuwa akikitamani ambapo kwa sasa tayari kimeshafanyiwa kazi ni kuongeza tozo kwa bidhaa za ngozi kutoka nje

Aliamini kwa kufanya hivyo idadi ya waagizaji itapungua lakini hata ambao wataingiza kwa kuwa ushuru ni mkubwa basi watauza na wao bei ghali

Lakini alienda mbali zaidi na kutamani tume ya ushindani nchini(FCC)itekeleze wajibu wake wa kisheria katika kuondoa bidhaa bandia sokoni lengo likiwa ni kunusuru viwanda vya ndani na ustawi wa taifa kwa ujumla wake.

HATIMAYE NDOTO IKATIMIA

Katika kuonyesha kwamba serikali ilisikia kilio hicho cha wazalishaji wazawa hatimaye wakaongeza ushuru katika bidhaa zinazotoka nje ambazo malighafi yake yanapatikana.

Hayo yalijiri katika uwasilishaji wa bajeti kuu ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa bungeni ambapo bidhaa zitokazo nje ikiwemo bidhaa za ngozi ni miongoni mwao maeneo ambayo tozo hiyo iliongezwa

Waziri wa fedha Dkt Mwigulu Nchemba alisema kwa kufanya hivyo kutawezesha kuponya viwanda vya ndani lakini pia kuvifanya vikue na kuongeza wigo wa ajira sanjari na pato la taifa kwa ujumla wake.

MWISHO

Leave a Reply