Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Vijana kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uongozi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa pamoja na utunzaji wa mazingira.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Miaka 102 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma. Amesema Maendeleo ya Taifa lolote duniani yanategemea vijana na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uongozi kama ambavyo Baba wa Taifa alivyofanya.
Amewahimiza Vijana kuendelea kuweka mkazo katika kupata elimu kama Mwalimu Nyerere alivyosisitiza elimu kama njia ya kupambana na umasikini. Amewataka vijana wote wa kitanzania kufanya jitihada za kuelewa misingi na faida za Muungano na kuwa mstari wa mbele katika kuulinda na kuuenzi muungano huo adhimu. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa vijana wa kitanzania kuelewa kuwa Tanzania ilishiriki ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika kwa kutambua kuwa uhuru na usalama wa Tanzania unategemea pia uhuru wa nchi nyingine za Afrika.
Makamu wa Rais amesema katika kumuenzi Baba wa Taifa aliyehimiza matumizi ya kiswahili katika kuwaunganisha watanzania wakati wa kupigania uhuru na baada ya kujitawala pamoja na kudumisha utamaduni wa mtanzania, hapana budi vijana wa kitanzania kutambua nafasi ya pekee kujivunia lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania. Amewataka kutumia fursa zilizopo katika lugha hiyo ikiwemo ukalimani, uandishi wa vitabu vya kiada na ziada na vitabu vingine, ufundishaji wa kiswahili katika nchi mbalimbali, tafsiri ya vitabu vya lugha nyingine kwa kiswahili na matumizi ya kiswahili katika sanaa na muziki.
Makamu wa Rais amehimiza Mamlaka za Hifadhi za Taifa na watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada za kulinda hifadhi na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo ili kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliweka mkazo katika kuhifadhi rasilimali za Taifa. Amewasihi watanzania kuwa wazalendo, kudumisha amani na kuepuka ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, itikadi za kisiasa au kabila kama ambavyo Mwalimu Nyerere alisisitiza wakati wote wa uhai wake.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuendelea kulinda, kutunza na kuhifadhi Malikale ikiwa ni pamoja na zilizokuwa nyumba na kambi za wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika hapa nchini. Aidha ametoa rai kwa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuangalia uwezekano wa kufanya kazi na wadau wengine kuangalia namna bora ya kuhifadhi kumbukumbu za Baba wa Taifa kama inavyofanyika kwa waasisi wa mataifa mengine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dastun Kitandula amesema kwa kutambua umuhimu wa kuhifadhi na kutangaza urithi wa Baba wa Taifa Mwal. Nyerere kutoka kizazi kimoja hadi kingine Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa mpango wa kitaifa wa miaka 10 wa kuenzi na kutangaza urithi huo kwa mwaka 2021/2022 – 2031/2032.
Aidha amesema mpango huo unalenga kukusanya na kuhifadhi na kutangaza urithi wa Mwalimu Nyerere, kujenga na kuboresha miundombinu stahiki katika maeneo yenye historia ya Mwalimu Nyerere, kuratibu na kushirikisha wadau katika kumuenzi Mwalimu Nyerere pamoja na kuendeleza tunu za Taifa zilizoasisi na Mwalimu Nyerere.
Naibu Waziri amesema tayari Wizara imepata kiwanja eneo la Chisinjili Jijini Dodoma kwaajili ya ujenzi wa Makumbusho ya Marais ambayo itakuwa na sehemu maalum ya historia na mchango wa Mwalimu Nyerere kitaifa na kimataifa.
Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mzee Paul Kimiti ametoa rai ya wananchi kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuhakikisha fikra zake zinaishi kwa vizazi vyote. Amewasihi Watanzania kuwa na ushirikiano katika kutekeleza masuala mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutatua changamoto.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miaka mitatu ya uongozi wake pamoja na Miaka 60 ya Muungano.