MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI PROFESA PATRICK NDAKIDEMI AONGOZANA NA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA PROF. MKENDA ALIPOTEMBELEA CHUO CHA UFUNDI STADI KIBOSHO.

Na Gift Mongi
Moshi

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi tarehe 31.07.2024 aliambatana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Adolf Mkenda (Mb) alipotembelea Chuo Cha Ufundi Stadi (Kibosho Vocational Traing Center – KVTC) kilichopo katika Kata ya Kibosho Magharibi, Tarafa ya Kibosho.

Katika ziara hiyo, walikuwepo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, Mwenyekiti wa bodi ya Chuo Filipina Ofunguo na Wajumbe wa bodi, Diwani mwenyeji Prosper Massawe, Madiwani kutoka Kata jirani za TARAFA ya Kibosho, wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Ofisi ya Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, waalimu na wanafunzi kutoka Shule jirani na Chuo cha KVTC.

Lengo kuu la ziara yao ilikuwa ni kujionea shughuli zinazoendeshwa na Chuo ambapo Prof. Mkenda alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo chuoni.

Alitembelea na kujionea Maabarara za TEHAMA, Ufundi Seremala na Ushonaji, miradi wa kilimo cha mbogamboga, mahindi, kahawa, kilimo cha parachichi, ufugaji wa ngombe, mbuzi, kuku na nguruwe.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo . Filipina Ufunguo alimshukuru Mh. Waziri kwa kutenga muda na kukitembelea Chuo cha KVTC.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Chuo ndugu Danieli Mboya alieleza kuwa Chuo kinakabiliwa na Changamoto mbalimbali zikiwemo ya Uchache wa wanafunzi, Wafadhili (kutoka Uholanzi) kujitoa kukisaidia chuo, Mwitikio mdogo wa wananchi wa TARAFA ya Kibosho kusaidia raslimali fedha za kukiendesha Chuo, ukosefu wa zana za kisasa za kufundishia, na chuo kushindwa kukamilisha ujenzi wa majengo pamoja na baadhi ya karakana kama ilivyokusudiwa.

Akitoa salamu zake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Boisafi alimshukuru Mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko wake wa kukitembelea Chuo cha KVTC. Pia aliwashukuru viongozi wote wa Chuo wakisimamiwa na bodi kwa jinsi wanavyofanya kazi kubwa ya kukiendesha chuo. Aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuipandisha hadhi Sekondari ya Somsom iliyopakana na KVTC.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi alimshukuru Mgeni rasmi kwa kuitembelea taasisi hiyo nyeti iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika jimbo lake.

Aliishukuru Serikali inayoongozwa na Dr Samia Suluhu Hassan kwa kulipatia jimbo la Moshi vijijini Shule mpya ya Sekondari ya Amali.

Alimwomba mgeni rasmi kuangalia uwezekano wa Serikali kuwalipa mishahara waalimu wa KVTC kwani Chuo kinakabiliwa na changamoto kubwa ya raslimali fedha baada ya wafadhili kutoka Uholanzi kujitoa.

Pia aliiomba serikali isaidie kuongeza idadi ya wanafunzi watakaopangwa kusoma KVTC kwani mazingira ya kusoma ni mazuri.

Kutokana na uwepo wa eneo kubwa la ekari 40 katika shule ya Sekondari ya Somsom, Mh. Ndakidemi aliiomba serikali ilitumie vyema eneo hili kwa kuanzisha kidato cha 5 na 6 na kuifanya shule hiyo kuwa ya mafunzo ya Amali.

Akizungumza na Wanafunzi, Wafanyakazi wa Chuo hicho na wageni waalikwa mara baada ya kukagua na kupokea salamu kutoka kwa watu mbalimbali, Prof Mkenda alisema mradi unaoendeshwa na Chuo hicho ni muhimu sana kwa wananchi wa Tarafa ya Kibosho na Taifa kwa ujumla kwani unapunguza changamoto ya kuwapatia utaalamu na maarifa vijana wa Kitanzania.

Alisema, amezipokea changamoto zilizoelekezwa kwake, na akawaelekeza wataalamu walioambatana naye wasaidiane kuzitatua.

Prof Mkenda aliwashauri wanafunzi waliokuwa katika mkutano huo kusoma kwa bidii haswa masomo ya sayansi kwani Serikali inawalipia bure kwa masomo ya elimu ya juu kwa waliofulu vizuri kidato cha sita.

Profesa Mkenda alisema, Samia Scholarship itagharamia kwa asilimia mia moja masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi watakaosoma shahada katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba.

Akitoa neno la shukrani, diwani wa Kata ya Kibosho Magharibi Mh. Prospa Massawe alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukitembelea Chuo cha KVTC.

Mwisho

Leave a Reply