Na Mwandishi wetu-KILIMANJARO
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameitaka jamii kupaza sauti kukemea vitendo vya ukatili vinavyotokea ili kuwa na jamii iliyo salama hasa kwa Wanawake na Watoto.
Mhe. Nderiananga aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake katika Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro alipotembelea Tarafa ya Ugweno na Usangi ambapo alisema kila mmoja ana wajibu wa kukemea vitendo vya kikatili vinavyoendelea katika maeneo yao.
Alisema kumekuwa na wimbi la udhalilishaji kwa watoto na watu wenye ulemavu akiitaka jamii kushirikiana kukomesha vitendo hivyo ili waweze kuwa watu wema na kutimiza ndoto zao.
“Niwaombe mama zangu na wananchi wa Mwanga, Tarafa ya Usangi tushirikiane kukomesha ukatili, mtoto wa mwenzio ni wako akifanyiwa ukatili usimuache kwa sababu hawa watoto ndiyo Taifa la kesho tunalolijenga pamoja na kuwathamini watu wenye ulemavu msiwanyanyapae,”Alisema Mhe. Nderiananga.
Pia aliwahimiza viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kwa waumini itakayosadia kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu na hatimaye elimu hiyo kutolewa katika maeneo yao yanayowazunguka.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo Wilaya ya Mwanga Bi. Mariana Sumari aliwakumbusha kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na kila Halmashauri itakayowasaidia kuanzisha biashara waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi katika familia zao na Taifa kwa ujumla huku akiwapongeza kwa kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili.
“Tutakapoanza utaratibu wa mikopo niwaombe msisite kuchukua mfanye shughuli zenu mjikwamue pamoja na kutambua rasilimali zinazowazunguka. Pia niwashukuru kwa kushirikiana kupiga vita ukatili na kuwajali watu wenye ulemavu tofauti na ilivyokuwa awali tulikuwa tukiwaficha ndani tukiamini ni aibu kuwa na mtoto mwenye ulemavu,”Alieleza Afisa huyo.
Aidha Afisa Tarafa ya Usangi Bwa. Misonge Silanda alimpongeza Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambapo alitoa zaidi ya shilingi Bilioni Tatu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, maji na miundombinu ya Barabara.
==MWISHO==