Na Mwandishi Wetu.
Moshi.Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa Vijana wa Chama cha mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi vijijini, mkoani Kilimanjaro, Yuvenal Shirima amewataka vijana kuacha kutengenezeana ajali za kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani na badala yake kila mmoja ajipange kuhakikisha anakitafutia chama ushindi.
Shirima ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao cha baraza la UVCCM wilayani humo, kilichofanyika katika msitu wa Rau, ambapo pia, amewataka vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, ili kuweza kupata fursa za kuingia kwenye vikao vya maamuzi kuanzia ngazi za vitongoji na vijiji.
Amesema huu si wakati wa kutengenezeana ajali za kisiasa wala kuwa na makundi, huku akihimiza umoja na mshikamano katika kukipigania chama ili kiweze kushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
“Ndugu zangu, tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, niwaombe vijana wote wenye nia na sifa za uongozi, tukajitokeze kugombea, ili tukapate nafasi ya kusemea changamoto za vijana katika maeneo yetu, lakini pia vijana tuache kutengenezeana ajali za kisiasa, kipindi hiki tuwe makini sana”.
Amesema “Vijana kwa sasa hatutaki makundi na mihemko isiyokuwa ya msingi, tukaonyeshe nguvu kazi tuliokuwa nayo ili watu wasiseme tu tunao vijana wa CCM, bali waseme wapo vijana nguvu kazi ya Taifa na linapotokea jambo, tukawajibu watu kwa hoja na tuepuke matusi, tusimtukane mtu, tusimame kwenye hoja”.
Amesema ni wajibu pia wa vijana kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura, ili kuwa na sifa ya kushiriki uchaguzi wakati utakapofika.
“Kila aliye katibu na mwenyekiti wa Kata na kamati yake ya utekelezaji ahakikishe anakwenda kushusha maelekezo kwenye matawi yote, vijana wote walioko kwenye eneo lake wakajiandikishe katika daftari la kudumu la mpiga kura, na kipimo cha uongozi ni hiki na siyo uende kilele mama”.
Aidha amewataka viongozi wa vijana kwenye kata kuweka mikakati ya ushindi na kwamba kwa yule ambaye anaona kazi hiyo haiwezi, apishe nafasi mapema.
“Viongozi nendeni mkajipange, kaonyesheni ukakamavu wa kutosha wa umoja wa vijana na tunapaswa kuweka mipango mikakati ya ushindi na ukiona huwezi kuweka mikakati mizuri ya kuhakikisha CCM inashinda wenyeviti wa vijiji na vitongoji mwaka huu anza sasa hivi kujiuzulu utupishe”.
Amesema “Kazi inayofanywa na serikali ni kubwa, hivyo vijana tunapaswa kuwa mabalozi kwenda kusema kazi zilizofanywa na zinazoendeleakufanywa na serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan na tuendelee kukipigania chama chetu”
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Pantaleo Melkiori amewaasa viongozi wa vijana kwenye kata, kuepuka kutumika vibaya kisiasa na kila mmoja kujipanga vyema na uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Ndugu zangu tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, ni wakati wetu wa kuendelea kujipanga vuzuri katika maeneo yetu, ili kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo wakati wa uchaguzi utakapofika”
Mwisho.