You are currently viewing MASOKO YA UHAKIKA YA BIDHAA ZA NGOZI TUNAYAHITAJI…

MASOKO YA UHAKIKA YA BIDHAA ZA NGOZI TUNAYAHITAJI…

Na Gift Mongi
MOSHI.

Wazalishaji wa bidhaa za ngozi nchini wamesema licha ya serikali kuondoa tozo kwenye bidhaa hizo bado kuna umuhimu wa kutafuta masoko ya uhakika nje ya nchi ili kuweza kuwasaidia wazalishaji hao sambamba na kuboresha matumizi ya bidhaa za ngozi hapa nchini.

Serikali ya nchini China tayari imeshafungua milango yake ambapo itawezesha bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania kuuzika katika nchi hiyo na hii inatokana na ziara iliyofanywa na rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika taifa hilo.

Kinyume chake imeonekana kuwepo kwa bidhaa bandia zenye mfanano na zile zenye kuzalishwa hapa nchni jambo linaloelezwa kuwa ni mwiba kwa viwanda vya ndani vyenye kuzalisha bidhaa za ngozi

Mkurugenzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Woisso Original Products(WOP)Kenneth Woisso alisema serikali imeweka jitihada mbali mbali katika kukuza soko la ngozi na kuwa ipo haja ya kutafuta masoko ya uhakika katika nchi hiyo ili kufanya biashara hiyo iweze kukua zaidi ya hapa ilipo kwa sasa.

Alisema kuuza bidhaa hizo kwa mtu mmoja mmoja bila kuwa na uhakika wa soko bado inaweza kuwa ni vigumu lakini kama zitatumika njia nyingine mfano ubalozi Tanzania kuunganisha wanunuzi na wazalishaji wa humu ndani biashara hiyo ingenda kuimarika zaidi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo ni kuwa nchi ya China ina uwezo mkubwa wa kimtaji na hivyo sisi kama wazalishaji ni vyema tukajipanga katika kutosheleza soko lao la uhitaji ili kukidhi mahitaji ya kila siku.

“Wenzetu wanajiweza kimtaji hivyo na sisi kama tunaenda kufanya nao biashara ni lazima tujipange kikamilifu maana kwanza hatuna uzoefu lakini hata mteja mwenyewe hatujui kwa kumpata”alisema

Aidha Woisso alisema bado ipo haja ya serikali kuendelea kuwashika wadau wa sekta ya ngozi mkono kwa kuwatafutia mtandao wa masoko ya nje kwani bado sekta hiyo haijaanza kufanya vizuri ndio kama inaanza kuchipukia.

Alisema kama biashara hiyo itaenda kukua na kufanya vizuri kama ambavyo ni dhamira ya serikali na hivyo basi hata wafugaji nao wataweza kunufaika kwani malighafi yanayotokana na mifugo itakuwa na soko la uhakika zaidi.

Kelvin Msaki ambaye ni muuzaji wa ngozi alisema kwa sasa biashara hiyo imeonekana kukumbukwa tofauti na ilivyokuwa kwa kipindi cha nyuma na kuwa jitihada hizo zikiendelea sekta hii itaenda kufikia mahali pazuri zaidi ya ilipo.

Alisema njia pamoja na mifumo inavyozidi kuimarishwa inaleta matumaini kwani kuna muda ulifikia biashara hiyo ikawa inahujumiwa sambamba na soko la ndani kudidimia kwa kiwango kikubwa.

Kwa kipindi cha miaka michache serikali imeweka jitihada za maksudi katika kufufua sekta ya ngozi ikiwa ni pamoja na kuongeza tozo kwa bidhaa za ngozi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Mwisho.

Leave a Reply