Na Mwandishi Wetu
Moshi.Umoja wa Vijana wa Chama cha mapinduzi, (UVCCM) Wilaya ya Moshi vijijini, imezindua operesheni ya tunazima zote tunawasha ya Kijani hadi mashinani, ikibeba malengo matano, ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama na kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura.
Operesheni hiyo ambayo imezinduliwa katika kata ya Mabogini, itafanyika kwenye kata zote 32 za wilaya hiyo, ambapo viongozi wa UVCCM wilayani humo wakiongozwa na mwenyekiti wake, Yuvenal Shirima watapita shina hadi shina kuzungumza na wananchi na kupeperusha bendera za chama hicho.
Akizungumza Shirima amesema opereresheni hiyo itamalizika Agosti 31 mwaka huu na kwamba wanatarajia kuongeza idadi ya wanachama na kuwasajili wengi zaidi katika mfumo wa kielektroniki.
“Leo tumezindua rasmi operesheni yetu ya tunazima zote tunawasha ya kijani hadi mashinani, na lengo la operesheni hii ni kusajili wanachama wapya ndani ya jumuiya ya vijana na ndani ya chama cha mapinduzi, ambapo imeanzia kata ya mabogini na tutapita shina kwa shina katika kata zote 32, kuzungumza na wanachama na wananchi kwa ujumla, na tutasikiliza kero na changamoto zinazowakabili, ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi”
Amesema katika ziara hiyo wanatembea na maofisa Tehama wa chama Wilaya ambapo katika Kata ya Mabogini tayati wamesajili wanachama zaidi 300 kielektroniki.
Amesema lengo la pili la ziara hiyo ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura wakati utakapofika ili kuwa na sifa na kupata haki ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.
“Lakini lengo la tatu ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini pia kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi sahihi ambao watasimama kuwatumikia na kushughulika na changamoto zilizopo katika maeneo yao”
Ameongeza kuwa “Lakini pia katika ziara hii tutaeleza kazi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan na jitihada za serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kutatua changamoto za wananchi”.
Aidha amesema wamepata pia fursa ya kusikiliza changamoto zinazowakabili mabalozi ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo kuendelea kukipigania chama hicho tawala nchini, ili kuhakikisha kinapata ushindi katika chaguzi zijazo.
Miongoni mwa changamoto ambazo zimetajwa na wananchi wa kata ya mabogini ni kukosekana kwa huduma ya maji safi na umeme kwa baadhi ya wananchi pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, ambapo Shirima aliahidi kuzibeba kwa ajili ya kuziwasilisha maeneo husika ili kuweza kutafutiwa ufumbuzi.
Baadhi ya wanachama wa CCM katika mashina yaliyotembelewa, wamepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa inaimarisha uhai wa chama.
“Kutembelewa na viongozi ni faraja sana, kwani wameweza kutembelea mashina mbalimbali kuzungumza na mabalozi na wananchi ambao wameelezea kero zao, hii ni moja ya jitihada za kuimarisha uhai wa chama”amesema Mwanaisha
Mwisho.