You are currently viewing MBUNGE NDAKIDEMI ATEMBELEA WAPIGA KURA WAKE KATA YA KIBOSHO KATI

MBUNGE NDAKIDEMI ATEMBELEA WAPIGA KURA WAKE KATA YA KIBOSHO KATI

Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi tarehe 15.07.2024 amefanya ziara ya kutembelea wananchi wa Kata ya Kibosho Kati. 

Mbunge Ndakidemi aliandamana na Diwani wa Kata hiyo Mh Bahati Mamboma, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi ndugu Ramadhani Mahanyu, viongozi wa Chama na serikali Kata, na wataalamu kutoka Tanesco na mlinzi wa Kata Mkaguzi Msaidizi wa jeshi la Polisi Johari. 

Katika ziara hiyo, Mbunge Ndakidemi alikagua mradi wa uboreshaji wa upatikanaji maji katika kijiji cha Uchau Kusini na vitongoji vyake ambapo serikali imetoa sh milioni 438,000,000.00.

Akimkaribisha Mbunge kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Uchau Kaskazini, Diwani wa Kata ya Kibosho Kati, Mh Bahati Mamboma alimshukuru Mbunge kwa ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwake.

Akiongea na wananchi, Prof. Ndakidemi aliishukuru serikali iliyo  chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta za Elimu, Kilimo, Ustawi wa Jamii, Miundombinu ya barabara, Maji, Afya na Umeme. Aliwaeleza wananchi kwamba kwa kipindi cha miaka minne, Kata ya Kibosho Kati imepata miradi yenye thamani ya sh. Bilion 2,225,509,424.00.

Wakiwakilisha kero zao, wananchi wengi walionyesha kukerwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa wakati wa kampeni.  Waziri Mkuu aliahidi kuwa serikali ingekamilisha barabara ya International School – Kwa Raphael – Kibosho Shine kwa kiwango cha lami baada ya uchaguzi. 

Kero ya Matumizi mabaya ya shamba la ushirika linalomilikiwa na wanaushirika wa Kimasio na Kirima Boro iliibuliwa katika mkutano huo na mzee James Lelo Massawe ambaye alisema kuwa viongozi wamekuwa na tabia ya kuuza shamba la ushirika kinyemela bila kushirikisha wamiliki jambo linalosababisha sintofahamu kubwa. Mwananchi huyu alimwomba Mbunge asaidie  kufuatilia na kuhakikisha shamba hilo linapimwa upya.

Katika kikao hicho vijana walionyesha uhitaji mkubwa wa mikopo iliyokuwa inatolewa na halmashauri.

Katika mkutano huo, Mh Mbunge aligawa miche ya kisasa ya migomba yenye uwezo wa kuzaa mikungu mikubwa.

Akijibu hoja za kero za wananchi, Mbunge aliahidi kuzifikisha katika mamkaka husika.

Akiongea katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ndugu Ramadhani Mahanyu aliwaomba wananchi wa Kibosho Kati waendelee kuiunga mkono Serikali ya Rais Samia  kwani makubwa anayofanya kwenye taifa hili na Kata ya Kibosho Kati yanaonekana. 

Akiwa anafunga kikao, Mwenyekiti wa  CCM Kata Edward Mallya amemshukuru Rais Samia kwa miradi mikubwa ndani ya Kata yao pamoja na kumshukuru Mbunge na Diwani kwa ushirIkiano mkubwa baina yao unaopelekea wananchi  kupata maendeleo.

Leave a Reply