You are currently viewing NAIBU WAZIRI UMMY ATAKA UHAMASISHAJI KWA WATU WENYE ULEMAVU KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUPIGA KURA..

NAIBU WAZIRI UMMY ATAKA UHAMASISHAJI KWA WATU WENYE ULEMAVU KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUPIGA KURA..

NAIBU Waziri Ofisi Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amewataka viongozi wa Umoja wa Waanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), kwa kushirikiana na viongozi wa Chama kuhamasisha watu wenye ulemavu kushiriki katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Ummy ametoa kauli hiyo wakati alipozungumza na viongozi wa UWT Tarafa ya Same, Chome suji na Mwembe mbaga katika jimbo la Same magharibi na kufuatiwa na mkutano wa hadhara katika kata ya Mwembe ambapo alisema kuwa, kwa sasa serikali imeweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu katika kujiandikisha.

“Viongozi wa Chama na Jumuiya zake tunao wajibu mkubwa wa kuwahamasisha watu wenye ulemavu kujiandikisha katika daftari la kupigia kura na kwa sasa tumeboresha sana ili kuendana na hali zao hivyo niwaombe msisite kujitokeza kujiandikisha” alisema Naibu Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaomba watu wenye ulemavu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu mwakani huku akiwataka viongozi wa CCM kuwaunga mkono watu hao.

Ummy alisema kuwa, wilaya ya Same ni ngome ya Chama cha Mapinduzi hivyo amewataka wanaccm pamoja na Wananchi kutokukubali kuchezewa na viongozi wa vyama vya upinzani na kuwasihi kushiriki kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura ili kupata fursa ya kutetea wilaya ya same kuendelea kuwa ngome ya ccm.

“Natambua bado zoezi la kujiandikisha katika daftari la kupigia kura halijafika Kilimanjaro lakini niwaombe viongozi wa chama changu endeleeni kuhamasisha wananchi ili pindi muda utakapofika washiriki kwa wingi kujiandikisha na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM” alisema Ummy.

Kwa upande wake, Katibu wa UWT mkoa wa Kilimanjaro, Irimina Mushongi amewataka wanawake kuhakikisha wanambeba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu mwakani.

Katibu huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wakinamama kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwachagua viongozi bora watakaowavusha katika maendeleo.

Alisema kuwa, wapo baadhi ya viongozi wa chama wameanza kuwabeba baadhi ya wanachama walioanza kutangaza nia za kugombea nafasi mbalimbali na kuwaonya kuacha tabia hiyo na badala yake watekeleze majukumu waliyopewa.

Mwisho..

Leave a Reply