ABC Impact yatoa baiskeli 300 kwa wanafunzi wa kike
NA KIJA ELIAS, MOSHI.
DIWANI wa Kata ya Mabogini Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Dk. Bibiana Massawe, amekabidhi baiskeli 300 kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekondari, ambao wanakabaliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu wa kilometa 10 hadi shuleni hali ambayo inapelekea baadhi yao kukatisha masomo kutokana na kupata ujauzito.
Diwani wa Kata ya Mabogini Bibiana Massawe, akikata utepe kuzindua ugawaji wa baiskeli zilizotolewa na Shirika lisilo kuwa la kiserikalo la ABC Impact
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi baiskeli zilizotolewa na Shirika lisilo kuwa la kiserikalo la ABC Impact Dk. Massawe amesema baiskeli hizo zitawasaidia watoto wa kike kufika shuleni kwa wakati na kuondokana na utoro wa mara kwa mara kutokana na umbali mrefu wanaotembea hadi kufika shuleni.
Aidha diwani huyo ametoa wito kwa mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kuwasaidia pia na vijana wa kiume, kwani kwa kuwaweka pembeni kunasababisha kujiingiza katika makundi yasiyo faa ikiwemo masuala ya ushoga.
Awali akizungumza Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Mpirani Remmy Kaganga, amesema mradi huo wa baiskeli umewanufaisha wanafunzi 476 huku asilimia 90 wakiwa ni mabinti wa kike na asilimia 10 wakiwa ni vijana.
“Wanafunzi hawa walikuwa wakitembea umbali wa kilometa 10 kwenda na kurudi, huku baadhi ya wanafunzi wa kike walikuwa wakipata mimba kutokana na vishawishi walivyokuwa wakivipata njiani,”amesema Mwl. Kaganga.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la ABC Impact Ayanna Kimaro, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi baiskeli 300 kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekondari wilaya ya Moshi na Hai
Naye Mratibu Elimu Kata ya Mabogini John Mariki, amesema matukio ya mimba za utotoni yanatishia usalama wa watoto wa kike, kutokana na kutembea umbali mrefu kufika shuleni wakiwa wamechoka jambo ambalo liliwasababishia hata ufaulu wao kutokuwa mzuri darasani.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la ABC Impact Ayanna Kimaro, amesema lengo la utoaji wa baiskeli hizo kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekonadri ni kuwapunguzia adha za usafiri wa kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Diwani wa Kata ya Mabogini Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Dk. Bibiana Massawe, akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea baiskeli 300 zilizotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la ABC Impact
“Leo tunagawa baiskeli 300 kwa shule za sekondari tano zilizopo Wilaya ya Moshi Vijijini na Wilaya ya Hai, ambapo mabinti wa kike wapatao 250 watapata baiskeli hizi na wanafunzi wa kiume wapato 50 na wao watakwenda kunufaika na mgao huu.”
Dkt. Bibiana
Wakielezea mchango wa baiskeli hizo namna zilivyo wasaidia baadhi ya wanafunzi hao Aureria Kokusima, Jesca Tesha na Mohammed Mstapha, wamesema, zitawasaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka changamoto zilizopo mbele yao na kwamba wataweza kuwahi shuleni, kufanya vyema kwenye masomo na kufaulu vizuri.
Shule zilizobahatika kupata mgao huo wa baiskeli kwa baadhi ya wanafunzi wa kike ni shule ya Sekondari Mabogini amabayo imepata baiskeli 60, TPC, Oria, Mpirani na shule ya Sekondari Kia Day iliyopo Wilaya ya Hai.
MWISHO.