Na Mwandishi wetu
Moshi.
Umoja wa vijana wa Chama cha mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi vijijini, umeanza kampeni ya ugawaji na uoteshaji wa miti katika vijiji vya kata ya Kirua vunjo kusini na maeneo jirani lengo likiwa ni kukabiliana na athari za mmomonyoko wa udongo na mabadiliko ya tabianchi.
Umoja huo umegawa miti kwa mabalozi wa nyumba 10 na taasisi za umma ikiwemo shule za msingi na sekondari ili kuchochea hamasa ya kampeni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuanzia ngazi za chini.
Akizungumza wakati wa ugawaji miche hiyo kwa mabalozi na taasisi za umma, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenali Shirima amesema moja ya athari ambazo zimesababishwa na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha ni mmomonyoko wa udongo.
Amesema wamepewa zaidi ya miche ya miti 3,000 na wakala wa Misitu Tanzwnia (TFS) Wilaya ya Moshi, ambayo wataigawa ili kuoteshwa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye vilima na maeneo ya kuzinguka vyanzo vya maji ili kupunguza kasi ya maji ambayo yanatokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Katika kipindi hiki cha mvua, kumekuwa na changamoto kubwa ya mmomonyoko ya udongo ambao umesababisha kuchimbika makorongo katika baadhi ya maeneo na ili kukabiliana na tatizo hili, tumeanza kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Moshi na leo tutagawa miti zaidi ya 3000 kwa mabalozi wa nyumba 10 na shule za msingi na sekondari” amesema Shirima na kuongeza kuwa
“Tunatambua mabalozi ndio viongozi ambao wako karibu zaidi na jamii, hivyo wakiihamasisha jamii kupanda miti na kutoa elimu jamii kubwa itapata uelewa, lakini pia tumekabidhi miti kwa shule za msingi na sekondari na kutaka wanafunzi wa shule hizo watunze miti hiyo ili kuwajengea uekewa na utamaduni wa kylinda na kutunza mazingira”.
“Tumepata ushirikiano mzuri kutoka idara ya misitu TFS ambao wametukabidhi zaidi ya miche ya miti 3000 ambayo tunaisambaza maeneo mbalimbali na tunatambua moja ya faida za kupanda miti ni kuepusha mmomonyoko wa udongo na tunapopanda miti kwa kasi tutaepusha adha hii katika vilima vyetu katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendekea kunyesha”.
Aidha amesema miti hiyo ni ya kivuli na rafiki katika kutunza mazingira na vyanzo vya maji na kwamba wataendelea kuhamasisha jamii ikiwemo vijana kulinda na kutunza mazingira yanayowazunguka.
Eden Jornas balozi namba nane Kata Kirua Vunjo Kusini, amesema mvua zinazonyesha zimesababisha makorongo katika maeneo mbalimbali na ili kukabiliana na athari hizo za mafuriko, kuna haja ya kuotesha miti kwa wingi.
“Hii miti tuliyopewa imekuja wakati muafaka kwani mvua zinazonyesha zimesababisha kuchimbika kwa makorongo mengi, sasa tutaenda kuipanda huko kwa wingi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuboresha mazingira na kudhibiti kasi ya mafuriko”.
Rukia Msangi kutoka kijiji cha Mabungo amesema bado miti inahitajika kuoteshwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na athari za mafuriko, ukame na hata mmomonyoko wa udongo.
“Tunaomba miti hii itolewe kwa wingi ili tuipande ya kutosha katika maeneo yetu na hata kwenye taasisi za umma kwani inasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo, ukame na hata upepo mkali”amesema Msangi.
Mwisho.