You are currently viewing Dkt. NCHIMBI SIONI MBADARA WA CCM

Dkt. NCHIMBI SIONI MBADARA WA CCM

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema hivi karibuni kumekuwa na majaribio ya watu kufikiri kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi au kila chama kinaweza kupewa nafasi ya kuongoza.

Amesema kwa sasa hakuna chama kinachoweza kupewa dhamana ya kuongoza nchi na watu wakapata usingizi zaidi ya Chama Cha Mapinduzi.

Nchimbi amesema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu ndani ya mkoa huo.

“Katibu wa Uenezi (Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makala) ameongea kwa kirefu yeye huwa anapiga moja kwa moja.

“Mimi Katibu Mkuu huwa ninazunguka kidogo. Kila mtu ana njia yake ya kufikisha ujumbe. Lazima tuendelee kukubaliana kwamba kwa sasa hakuna chama kinachoweza kupewa dhamana ya kuongoza nchi yetu na watu wakapata usingizi zaidi ya Chama Cha Mapinduzi.

“Kuna vitu ambavyo mtu haitaji kuambiwa, mnasikiliza redio, mnaangalia runinga, na mitando ya kijamii mnasikia viongozi wakubwa wakituhumiana wenyewe kwa wenyewe.

Anasema hapo wamekaa kwenye upinzani kwa miaka 20, huku watanzania wakiwapa muda wakomae.

“Waache kidogo wakomae na watanzania wamefika mahali wamefikiri sasa wenzetu wameanza kukomaa na mara wameanza kutukanana.

“Wakati mwingine tusikasirike tuwape muda, tuliwapa miaka 20 tumeona bado tuwape miaka 20 mingine tuwatazame tena inaweza kutoa nafasi ya kukomaa zaidi. Kwa sasa Chama Cha Mapinduzi kiendelee kupewa dhamana ya kuendesha nchi,” amesema.

Balozi Nchimbi amesema CCM kimedhibitisha kinao watu wanaoweza kuongoza, kinaweza kuweka mipango inayoweza kutekelezeka, kusimamia mipango yake na kuchagua viongozi kila baada ya miaka mitano wanaobadilisha safu ya uongozi.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, amemjibu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kwamba pikipiki zinazogawiwa ni za CCM.

“Jana nimemsikia Lissu anasema Rais Samia (Suluhu Hassan) amehonga pikipiki nchi nzima. Hiki ni Chama Cha Mapinduzi na Mama Samia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa na hiyo yote Lissu anavyotaja tumegawa pikipiki anaeleza uimara wa CCM kwamba, kimejipanga kushinda uchaguzi ujao,” amesema.

Anasema pikipiki anazoeleza ni za Chama Cha Mapinduzi na kushukuru (wapinzani) wameanza kutapatapa na yeye (Lissu) ameanza kuonesha uimara wa CCM.

“Sasa kama wewe baiskeli huna alafu ushindane na CCM. Ninataka kumwambia pikipiki hizo ni za Chama Cha Mapinduzi zimetolewa, na Katibu Mkuu ameeleza vizuri kwenye mkutano wa ndani ya kwamba, ni vitendea kazi asipotoshe watu kwamba, watu wamehongwa pikipiki.

“Wao ndio wanaotoa rushwa, alisema yeye mwenyewe (Lissu) wana fedha chafu kazi kwao, sisi tumetoa vitendeka kazi kwa chama,” amefafanua

Leave a Reply