Dokta Saleh bin Zainul Abedin Al Shebi, mtunzaji wa funguo za Kaaba ama Al-Kaaba, eneo takatifu zaidi kwa Waislamu, amefariki dunia.
Inaaminika familia yake ilipata ufunguo huu wakati wa Mtume Mohammad na imekuwa na ufunguo huo tangu wakati huo.
Kwa karne nyingi, familia ya Dk. Sahel bin Zainul Abedin imebeba jukumu la kuuweka ufunguo huo salama. Dk. Saleh alikuwa mrithi wa 109 wa familia ya Al Shebi, aliyepewa jukumu la kutunza ufunguo huo.
Ufunguo ulikabidhiwa kwa Dk. Saleh baada ya kifo cha mjomba wake Abdul Qadir Taha Al Shebi 2013.
Dk. Saleh, aliyesoma PhD yake ya Masomo ya Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Umm Ul Qura, alizaliwa katika jiji la Makka mwaka 1947. Mekka inachukuliwa kuwa jiji takatifu zaidi katika Uislamu.
Alifundisha akiwa mhadhiri katika chuo kikuu hicho kwa miaka mingi. Pia alichapisha makala nyingi za utafiti na vitabu vinavyohusiana na Uislamu.
Historia ya ufunguo wa Al-Kaaba
Kuna mlango mmoja tu wa kuingia Al-Kaaba ambao unaitwa Bab-e-Kaaba.
Al-Kaaba ina urefu wa mita 2.13 kutoka sakafu ya Msikiti wa Al-Haram. Mlango upo karibu na ukuta wa kaskazini-mashariki wa Al-Kaaba na upo karibu na jiwe jeusi mahali ambapo Tawaf inaanzia.
Wakati wa Hajj au Umrah, mahujaji hubusu jiwe jeusi na kisha huizunguka Al-Kaaba katika ibada inayoitwa tawaf.
Mwanahistoria wa Kiislamu Ahmed Adan, alizungumza kuhusu historia ya funguo za Al-Kaaba, anasema:
“Wakati Mtume Muhammad alipozaliwa, majukumu ya ukoo wa Maquraishi yaligawanywa. Familia ya Bani Hashim, ya Mtume, ilisimamia kisima cha Zamzam na na ufunguo wake. Huku ufunguo wa Al-Kaaba ukitunzwa na Usman bin Talha.”
Ahmed Adan anaelezea tukio ambalo Mtume Muhammad alimwambia Uthman bin Talha, ‘siku inakaribia ambapo nitapata ufunguo huu.’
Kwa mujibu wa historia ya Kiislamu, baada ya kutekwa Makka, ufunguo huu ulichukuliwa kutoka kwa Uthman bin Talha, lakini kisha ulirudishwa kwake kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Mtume Mohammad mwenyewe alimpa Usman bin Talha ufunguo huu, na tangu wakati huo familia yake imekuwa ikiutunza kutoka kizazi hadi kizazi.
Inaelezwa kuwa Mtume Muhammad, alipokuwa akimpa Usman ufunguo, alisema, “ufunguo huu wa Al-Kaaba utabaki kwako na hakuna mtu atakayeweza kuuchukua isipokuwa mtu dhalimu.”
Ujenzi wa Mlango wa Al-Kaaba
Mlango wa Al-Kaaba
Kabla ya mwaka 1942, historia haielezi kuhusu nani alijenga mlango wa Al-Kaaba na jinsi ulivyojengwa.
Mwaka huo, ndipo Ibrahim Badr alijenga mlango wa fedha. Na mwaka 1979, mtoto wa Ibrahim, Badr Ahmed bin Ibrahim Badr alijenga mlango wa dhahabu kwa ajili ya Al-Kaaba. Mlango huu ulitengenezwa kwa kilo mia tatu za dhahabu.
Wakati Sheikh Abdul Qadir, akiwa mtunzaji wa funguo za Al-Kaaba, kufuli za Al-Kaaba zilibadilishwa kwa amri ya Mfalme Abdullah.
Mwanamfalme wa wakati huo Khalid Al Faisal, alikabidhi kufuli mpya na ufunguo kwa Sheikh Abdul Qadir kwa niaba ya Mfalme Abdullah katika hafla ya kusafisha Kaaba.
Sheikh Abdul Qadir alipofariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, Dk. Saleh bin Zainul Abedin Al Shebi akawa mtunzaji mpya wa ufunguo huu.
Kufuli na funguo za Al-Kaaba zimebadilishwa mara nyingi na watawala wengi katika historia. Kwa kawaida funguo na kufuli za Al-Kaaba huchongwa na kuandikwa aya za Quran.
Katika miaka ya hivi karibuni, jukumu la mlinzi wa funguo za Al-Kaaba limekuwa tu kufungua na kufunga kufuli.
Lakini wageni wa serikali wanaotembelea Saudi Arabia, Ofisi ya Kifalme ya Saudi Arabia, Wizara ya Mambo ya Ndani au vikosi vya dharura vinaweza kufungua kufuli hii kwa ufunguo huo.
Fauka ya hilo, kila mwezi kumi na tano Muharram katika kalenda ya Kiislamu, kwa amri ya kifalme, watunza funguo hufungua mlango ya Kaaba ili Al-Kaaba iweze kusafishwa.
Kufuli na ufunguo wa Al-Kaaba
Kufuli na ufunguo wa sasa wa Kaaba umetengenezwa kwa dhahabu na kemikali za nikeli. Wakati ukanda wa ndani wa Kaaba una rangi ya kijani kibichi. Aya za Quran pia zimeandikwa kwenye kufuli na ufunguo.
Nchini Uturuki, jumba la makumbusho lina funguo 48 ambazo zilitumiwa na magavana wa wakati huo wa Dola la Ottoman kufungua Al-Kaaba.
Nchi ya Saudi Arabia hutunza matoleo ya kuchonga ya funguo hizo zilizotengenezwa kwa dhahabu safi.
Ufunguo wa Al-Kaaba uliotengenezwa katika karne ya 12 ulipigwa mnada mwaka 2008 kwa dola za kimarekani milioni 181.
Ufunguo huu ulinunuliwa na mnunuzi asiyejulikana wakati wa mnada wa vitu vya sanaa kutoka ulimwengu wa Kiislamu huko London.
Funguo za Al-Kaaba ambazo zilipigwa mnada zilitengenezwa kwa chuma na zilikuwa na urefu wa inchi kumi na tano.
Imeandikwa kwenye ufunguo huo – ‘umetengenezwa mahususi kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.’
Ufunguo huo ndio ufunguo pekee ambao unamilikiwa na mtu binafsi. Kando na hayo, funguo 58 za Al-Kaaba ziko katika makumbusho mbalimbali.