You are currently viewing DKT MPANGO AFIKA NYUMBANI KWA RAS KILIMANJARO KUHANI MSIBA

DKT MPANGO AFIKA NYUMBANI KWA RAS KILIMANJARO KUHANI MSIBA

Moshi. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewasili nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Tixon Nzunda (56) aliyefariki kwa ajali ya gari pamoja na dereva wake jana mkoani Kilimanjaro.

Nzunda akiwa na dereva wake, Alphonce Edson (54) walifariki jana Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari ilitokea saa 8:30 mchana katika eneo la Njia Panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Gari la aliyekuwa RAS Kilimanjaro, Tixon Nzunda baada ya kupata ajali jana Juni 18, 2024 eneo la Njia Panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Makamu huyo wa Rais, amewasili nyumbani hapo eneo la Shanty Town mjini Moshi saa 6:40 mchana akitokea mkoani Arusha

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana usiku na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Simon Maigwa chanzo ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari aina ya Scania mali ya Orange Gas kushindwa kulimudu gari lake na kwenda kugonga gari la RAS na kusababisha vifo hivyo papo hapo

Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda enzi za uhai wake.
Mpaka sasa ratiba ya mazishi ya Tixon hazijatolewa na kwamba inatazamiwa kutolewa muda mfupi ujao na Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu.

Leave a Reply