TULIANZA PAMOJA TWENDE PAMOJA …PROF NDAKIDEMI
Na Gift Mongi
Moshi
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi mapema alikagua miradi mitatu ya maendeleo na kufanya mkutano wa hadhara Katika Kijiji cha Kirima Kati, Kata ya Kibosho Kirima.
Katika ziara hiyo, Mbunge aliandamana na Katibu wa Wazazi Wilaya ya Moshi Vijijini ndugu Andrew Mwandu, Diwani wa Kata hiyo Mh Inyasi Stoki Mushi, Diwani wa Viti Maalumu Mh Aurelia Mwacha na Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Kibosho Kirima.
Mbunge alikagua miradi ya ujenzi wa kituo cha kuhifadhi zao la ndizi katika soko la Mkoringa, zahanati iliyoko Ngirini katika kijiji cha Kirima kati na Daraja la Kitara Kya Mburu linalopakana na kitongoji cha Kidachini na kijiji cha Boro Chini.
Katika mkutano wa hadhara, Mbunge Ndakidemi aliwasilisha ripoti ya kina ya miradi iliyotekelezwa kwenye Kata ya Kibosho Kirima kwa kipindi cha miaka minne iliyopita yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilion mbili ambapo wananchi walionyesha kuridhika sana. Pia Mbunge aliwaasa wananchi waachane na mpango Batali wa kutaka kujigawia shamba la Ushirika la Kirima Boro, kwani taratibu za Ushirika hazitaruhusu jambo hilo lenye lengo la kuua Ushirika wa Wananchi.
Vilevile, Mbunge aliwashauri wananchi wote washirikiane kikamilifu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kuboresha daftari la wapiga kura katika Kata ya Kibosho Kirima watakapitakiwa kufanya hivyo.
Katika mkutano huo, wananchi waliwakilisha kero chache. Kero hizo ni pamoja na ile ya kukamilisha kwa kiwango cha lami barabara ya International School – Kibosho KNCU – hadi kwa Rafaeli.
Wananchi pia walieleza kero kubwa ya ubovu wa mifereji mingi ya asili inayosababisha kukosekana kwa huduma ya maji ya kumwagilia mazao yao ya kahawa na migomba. Wananchi wamedai kuwa kukosekana kwa maji ya kumwagilia kumesababisha kuchelewesha maendeleo katika vijiji vya Kata ya Kibosho Kirima. Kero nyingine ilikuwa ni ile ya upatikanaji wa mikopo kwa makundi maalumu.
Akijibu hoja na kero za wananchi, Mbunge aliwashukuru sana wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa jinsi wanavyoshirikiana naye na Diwani kutekeleza miradi na kutatua kero za wananchi. Alisema ni jukumu lake na viongozi wenzake kutafuta majibu ya kero zao na kuzipeleka sehemu husika.
Kuhusu kero ya barabara, Mbunge alisema, Serikali imekuwa ikitenga fedha za kukarabati barabara ya International School – Kibosho KNCU – hadi kwa Rafaeli kwa kiwango cha changarawe kama alivyoeleza kwenye ripoti yake. Aliwaahidi wananchi kuwa ataendelea kuikumbusha serikali itimize ahadi ya kukamilisha hiyo barabara kwa kiwango cha lami.
Akiwajibu wananchi kuhusiana na hoja ya maji ya kumwagilia kahawa na migomba, Mbunge alimwomba Diwani wa Kata Mh Inyasi Stoki washirikiane ili kutafuta suluhu ya kero hiyo.
Kuhusiana na mikopo, Mbunge alishauri makundi yote maalumu washirikiane na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ili asaidie vikundi vyote vya Kata (vijana, akina mama na walemavu) vipate mikopo, kwani serikali imefungua hilo dirisha.
Mwishoni Mbunge aligawa miche bora ya migomba ambapo Wenyeviti watatu wa Vijiji walipokea miche kwa niaba ya wananchi wao. Pia Mwenyekiti wa CCM Kata alipokea miche ya kuwagawia viongozi wenzake wa CCM.
Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa kijiji ndugu Patrick Chuwa alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea, na aliahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.